Share news tips with us here at Hivisasa

Usalama umeimarishwa katika viwanja vya ndege humu nchini baada ya tetesi kuibuka kwamba huenda kundi la kigaidi la al-Shabaab linapanga kufanya mashambulizi katika viwanja hivyo.

Inadaiwa kwamba kundi hilo linalenga viwanja vya ndege vikuu hapa nchini ikiwa ni pamoja na Jomo Kenyatta Nairobi, Wilson Nairobi na kiwanja cha Moi mjini Mombasa.

Mamlaka ya ndege hapa nchini KAA imesema kuwa imeimarisha usalama zaidi katika viwanja vyake baada ya tetesi hizo kuibuka.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi mjini Mombasa hutegemewa zaidi katika safari za kila siku ambapo pia idara ya polisi imeimarisha usalama zaidi.

Kulingana na taarifa kutoka katika mamlaka ya huduma za ndege nchini siku ya Jumatatu ni kwamba kundi hilo linalenga safari za ndege za ndani kwa ndani ambapo watu wengi husafiri katika shughuli za kila siku.

Habari hizi zinakuja siku moja baada ya Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinet kukiri kwamba bado kundi hilo la al-Shabaab ni tishio humu nchini.

Hata hivyo, Inspekta Boinet aliwahimiza Wakenya kuwa makini na kutoa taarifa kwa polisi wanaposhuku jambo lolote linaloweza kuharibu usalama.

“Mwananchi yeyote anayeshuku au kuwa na wasiwasi anafaa kupiga simu na sisi kama polisi tutachukua hatua mara moja. Na hiyo ndio sababu mnaona kwamba tumepiga hatua hadi kufikia sasa,” alisema Boinet.

Tangu kundi hilo kuanza kutekeleza mashambulizi humu nchini, kumekuwa na wasiwasi kwamba huenda linalenga maeneo yenye idadi kubwa ya watu hususan maeneo ya mjini.