Share news tips with us here at Hivisasa

Usalama umeimarishwa katika mji wa Nakuru na viungani mwake, siku mbili kabla ya sherehe za Krisimasi. 

Kwa sasa kunashuhudiwa ongezeko la wasafiri wenye pilka pilka wengi wanaoelekea manyumbani mwao kutoka mijini.

Doria zimezidishwa mjini Nakuru, huku polisi wengine wakiwa na nguo za raia na wengine waliovalia sare zao rasmi.

Aidha polisi wa AP na wa kawaida wamewekwa katika maeneo ambayo kwa kawaida hushuhudia ongezeko la watu msimu huu wa sherehe, ikiwemo maduka ya jumla, vituo vya matatu na kwenye mabenki.

“Hakuna afisa hata mmoja wa polisi tunaruhusu awe kwenye mapumziko hadi Januari. Wahalifu wanaweza kuchukua nafasi kama hii kusababisha uhalifu kama wa Al-shabab, na kwa hivyo ni lazima kila afisa awe kazini,” alisema naibu OCPD Janet Wasike, alipohojiwa na mwandishi huyu kuhusu mikakati waliyoweka ya kuhakikisha usalama kabla, wakati na baada ya Krisimasi.

Kati ya mikakati hiyo ambayo pia inashirikisha idara ya trafiki, ni kuhakikisha magari yanabeba idadi ya abiria wanaostahili kisheria, kufanya doria mjini, pamoja na kuharibu mahandaki ya pombe haramu na kukamata walevi.