Idara ya usalama katika eneo la Pwani imewahakikisha wakaazi usalama dhabiti licha ya kuwepo na tishio la shambulizi la kigaidi nchini.
Mshirikishi mkuu wa utawala katika eneo la Pwani Nelson Marwa amesema kuwa maafisa maalum wa kitengo cha kukabiliana na magaidi wametumwa kushika doria kila mahali katika eneo la Pwani, hasa katika viwanja vya ndege, maeneo ya burudani, vituo vya basi ili kuhakikisha kuwa usalama unaimarisha.
Kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, katika makao makuu ya idara ya usalama, Marwa alisema kuwa maafisa wa usalama wako macho na watahakikisha kuwa hakuna mtu yeyote ama kundi lolote la kihalifu linavuruga usalama katika eneo la Pwani.
Marwa alionya kuwa atakayepatika akijaribu kuzua vurugu ama hofu miongoni mwa wakaazi atakabiliwa kisheria.
Aliwataka wakaazi kushirikiana kwa karibu mno na maafisa wa usalama katika kutoa habari kuhusu washukiwa wa ugaidi, ili waweze kukabiliwa kisheria.
"Idara ya usalama katika eneo la Pwani iko macho na maafisa wetu wako kila mahali kuhakikisha kuwa usalama unaimarishwa licha ya kuwa na tishio la kutokea kwa shambulizi la kigaidi nchini,” alisema Marwa.
Kuali ya Marwa inajiri baada ya Inspekta Jenerali mkuu wa polisi nchini Joseph Boinnet kutoa tahadhari kwa wananchi kuwa huenda wanamgambo wa al-Shabaab wakafanya mashambulizi ya kigaidi nchini kufuatia wanajeshi wa KDF kumiliki ngome zao kuu nchini Somalia.