Mshirikishi mkuu wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa amewataka watalii wa humu nchini sawia na wale kutoka mataifa ya kigeni kuondoa hofu za kiusalama wanapozuru maeneo ya Pwani.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Marwa amesema kuwa mikakati kabambe imewekwa ili kuhakikisha wakaazi sawia na wageni wanaozuru kaunti mbali mbali za Pwani hawatatiziki kwa lolote lile.

Akizungumza siku ya Jumatatu katika kikao na maafisa kutoka idara mbali mbali za kiusalama, Marwa alisema kuwa idadi ya walinda usalama imeongezwa kutokana na kuongezeka kwa wageni wanaozuru fuo za bahari na sehemu mbali mbali za kujivinjari.

“Usalama umeimarishwa vilivyo na maafisa wako tayari kukabiliana na yeyote yule anayetaka kuvuruga hali ya utulivu,” alisema Marwa.

Aidha, mshirikishi huyo amedokeza kuwa vikosi mbali mbali viko tayari kukabiliana na watovu wa usalama, hasa katika mipaka ya kaunti hizo za ukanda wa pwani.

Hata hivyo, amewasihi wakaazi kuwa waangalifu na kushirikiana katika kutoa taarifa muhimu kwa vyombo vya kiusalama.