Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki amewataka vijana mjini humo kushirikiana na idara ya usalama ili kuvikabili visa vya utovu wa usalama vinavyoshuhudiwa katika baadhi ya mitaa ya Mombasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika hafla ya kutoa hamasisho kwa vijana iliyoandaliwa katika ukumbi wa Tononoka mjini Mombasa siku ya Jumatano, Achoki alisema kuwa ushirikiano kati ya maafisa wa polisi na umma utasaidia kuimarisha usalama mjini humo.

“Tukishirikiana kama watu wa jamii moja, tukizungumza lugha moja, nawaahidi tutavitokomeza visa hivi vya watu kuvamiwa kiholelaholela kila mara,” alisema Achoki.

Aidha, kamishna huyo aliwahimiza vijana na jamii kwa jumla kutoa taarifa muhimu kwa idara ya usalama ikiwemo kuyataja majina ya vijana wanaohangaisha watu katika maeneo ya Mtopanaga na Barakani eneo bunge la Kisauni.

Kwa upande wake mwenyekiti wa shirika la ‘Kenya Community Support Center’ (KECOSCE), Phillis Mwema, aliwahimiza vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa kipindi hiki ambapo taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu wa 2017.

“Kwa mara nyingi vijana tunatumiwa sana na viongozi wa kisiasa kwa manufaa yao. Tafadhali safari hii tujitahadhari na viongozi kama hao,’’ alisema Mwema.

Aidha, aliwahimiza vijana wajitenge na makundi ya uhalifu na badala yake wajihusishe na masuala yatakayowasaidia katika maisha yao ya kila siku.