Ili kuimarisha viwango vya elimu katika eneo la Changamwe, ni lazima wazazi, walimu na wanafunzi washirikiane ili kujadili kwa kina maswala ya elimu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa Wadi ya Kipevu katika bunge la Kaunti ya Mombasa Ibrahim Kondo amesema kuwa viwango vya elimu katika maeneo mengine ya nchi vimepigwa jeki kutokana na ushirikiano miongoni mwa wakazi.

Akizungumza katika wadi yake, siku ya Jumamosi, Kondo alisema kuwa wazazi wengi wamekwepa majukumu yao na kushindwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao pindi wanapokuwa shuleni, na akasema kuwa hali hiyo inayorudisha nyuma viwango vya elimu.

“Lazima wazazi, walimu na wafunzi kushirikiana ndio maswala ya elimu yatapewa kipau mbele kwani wengi wa wazazi wamekwepa majukumu yao na kuchangia matokeo duni kwa wanafunzi,” alisema Kondo.

Kondo amewakosoa wazazi kwa kuwa wepesi wa kuwalaumu walimu pindi watoto wao wanapofanya vibaya masomoni ilhali ni kutokana na uzembe wa wazazi.