Waziri wa Utalii Najib Balala amesema kuwa sekta hiyo imeimarika kwa asilimia 14 katika kipindi cha miezi sita kutokana na juhudi za wadau.
Akizungumza katika kongamano la wadau wa sekta ya utalii katika Ikulu ya rais mjini Mombasa siku ya Jumatano, Balala amesema kuwa tayari serikali imetenga shilingi bilioni 1.5 kuboresha sekta hiyo kupitia Bodi ya Utalii nchini.
Balala alisema kuwa shilingi bilioni 100 zimetengwa kuboresha miundo msingi hasa barabara ya Dongo Kundu na Mavueni, ili kuhakikisha kuwa sekta ya utalii inakuwa kwa kasi hata katika saula la uchukuzi.
Aidha, amedokeza kuwa serikali ina mikakati ya kutenga hekari elfu 10 kujenga hoteli katika eneo la Pwani, kama njia moja wapo ya uwekezaji na kuwavutia watalii.
"Tumetenga fedha za kutosha katika sekta hii kuhakikisha kuwa tunaiimarisha zaidi sawia na kukabiliana na changamoto zilizopo kwa sasa,” alisema Balala.
Akigusia suala la usalama, Balala alisema kuwa serikali imeweka mikakati mwafaka hasa kupitia idara za usalama nchini, kuhakikisha kuwa magaidi na wahalifu wanakabiliwa vilivyo na kuondoa hofu ya watalii kutozuru humu nchini.