Wakazi mjini Molo wanaendelea kulalamikia huduma duni za afya zinazotolewa katika Hospitali ya Wilaya Molo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi hao sasa wamemtaka Gavana wa Jimbo la Nakuru Kinuthia Mbugua kuwachukulia hatua wahudumu wote wa afya ambao wamezembea kazini badala ya kusaidia wagonjwa ambao huenda hospitali hiyo kutafuta matibabu.

Wakaazi hao wamesema kuwa licha ya uwepo wa foleni kubwa ya wagonjwa ambao wanasubiri kutibiwa, madaktari, pamoja na wahudumu wa afya huonekana wakiwa ndani ya afisi zao bila shughuli maalum.

Familia moja ambayo mtoto wao mwenye umri wa miaka 11 alifariki kabla ya kupata matibabu, wamesema huenda mtoto huyo angenusurika kifo iwapo angepata huduma za matibabu ya dharura mara moja kutoka kwa wahudumu hao.

Mamake mtoto huyo alisema mwanao aligongwa na gari aina ya Nissan Matatu kwenye barabara ya Mau Summit kuelekea Total hatua chache tu kutoka nyumbani mwao.

Amesema licha ya kusababisha ajali, dereva wa gari hilo alitoweka katika ajali hiyo ya mwendo wa saa moja jioni. Mama huyo alieleza jinsi alivyofanya hima kunusuru maisha wa mtoto wake, lakini akapoteza maisha yake wakiwa bado anasubiri kwenye mlolongo wa wagonjwa waliokuwa kwenye foleni kwa muda mrefu bila kuhudumiwa.

Visa vya wauguzi katika hospitali hiyo kuwapuuza wagonjwa vimeendelea kuripotiwa kila kuchao huku waadhiliwa wakiitaka Serikali kuingilia kati na kutatua utepetevu huo.

Aidha wakaazi wa Wilaya Molo wamesema hali huwa mbaya hasa nyakati za usiku ambapo wanaotafuta matibabu katika hospitali hiyo hukesha usiku kucha huku wakielezwa kwamba hamna daktari wa kuwahudumia kwa zamu ya usiku.