Katibu mkuu wa baraza la Maimamu na wahubiri nchini Sheikh Mohammed Khalifa (kulia). [Picha-NMG]
Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini limewaomba viongozi na wakenya wote kuungana kwa ajili ya uwiano nchini baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuteua baraza lake la mawaziri.
Wakizungumza siku ya Jumamosi wakati wa ufunguzi wa tawi la Maimamu eneo la Taveta, viongozi hao wakiongozwa na katibu mkuu wa Maimamu Sheikh Mohammed Khalifa, walisema kuwa uteuzi ambao kiongozi wa taifa alifanya ulihusisha sura yote ya taifa la Kenya.
Khalifa aliwaomba wakenya wote kwa ujumla kusonga mbele kwa ajili ya maendeleo baada ya uteuzi huo.
“Sasa Rais ametaja baraza lake la mawaziri, tunahitaji kukoma kuingiza siasa katika swala hili na kuungana pamoja kama wakenya na kuzingatia maendeleo,’’ alisema Khalifa.
Sheikh khalifa aliongeza kuwa uchaguzi umeisha na kuwasihi wakenya wenzake kukumbatia amani na kujiepusha na siasa za mgawanyiko.
‘‘Sisi sote ni wakenya. Ningewasihi wakenya wenzangu kuishi kwa pamoja na kuzingatia masuala muhimu kama kusaidia watoto kutoka familia maskini kuenda shuleni, kujishughulisha na ukulima na viwanda, masuala ambayo yataboresha uchumi wetu,’’ aliongeza Khalifa.
Baraza hilo pia lilimshukuru rais Kenyatta kwa kuwateua waisilamu wanne katika baraza jipya la mawaziri.
Katika baraza jipya la mawaziri, Amina Mohammed ameteuliwa kuongoza wizara ya Elimu, Najib balala akisalia katika wizara ya Utalii, Aden Mohammed akisalia katika wizara ya viwanda huku Rashid Mohammed akiteuliwa kuongoza wizara ya michezo.