Kamati ya Halmashauri ya Bandari KPA imesema kwamba hakutakuwa na vikwazo katika zoezi la kumchagua mkurugenzi.
Akiongea na wanahabari siku ya Jumatano, mwenyekiti wa kamati hio Bw Marsden Madoka alisema kuwa zoezi hilo ni jukumu la bodi hiyo.
Hapo awali, kaimu mkurugenzi wa KPA Bi Catherine Wairi alikiri kuwepo kwa uhaba wa wafanyikazi huku idadi ya wafanyikazi katika bandari hiyo ikiripotiwa kuwa takribani 7000.
Aliyekuwa mkurugenzi mkuu katika Bandari ya Mombasa Bw Gichiri Ndua alikuwa miongoni mwa wafanyikazi wa ngazi za juu walioachishwa kazi kwa tuhma za kujihusisha na ufisadi mapema mwezi Februari.
OCPD wa bandari hiyo na kiongozi wa kitengo cha ujasusi wa Kaunti ya Mombasa pia walikuwepo miongoni mwa wakuu walionyeshwa mlango.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kamati maalum iliyoundwa na Rais Uhuru Kenyatta kushughulikia maswala yanayoathiri utendakazi katika Bandari ya Mombasa.
Kumekuwa na shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasi kutaka nafasi ilioachwa na Bwana Ndua kujazwa na mtu mwenye asili ya Pwani.
Aidha, wakaazi wa Pwani wamekuwa wakilalamikia nafasi chache za ajira wanazopewa katika Bandari hio huku wakiamini kuwa wanastahiki nafasi zaidi.