Utingo mmoja wa lori alifariki baada ya kukanyangwa na lori lililokuwa likisafirisha mawe ya ujenzi katika eneo la Shrine, Kijabe katika kaunti ndogo ya Subukia Jumatatu adhuhuri.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwa mjibu wa mkuu wa polisi katika eneo la Subukia Alex Ng’ang’a, utingo huyo alifariki papo hapo baada ya kukanyangwa na lori hilo wakati dereva wake alipokuwa akilirudisha nyuma ili kutoa mawe yanayo nuiwa kutumika katika ujenzi wa kanisa katika eneo hilo la Shrine.

Ng’ang’a alisema kondakta huyo, aliyefahamika kama James Ndegwa, wa miaka 30, aliruka kutoka kwa lori hilo wakati dereva alipokuwa akilirudisha nyuma.

“Kwa bahati mbaya mwendazake aligongwa na mlango na kuanguka chini na gurudumu la mbele likamkanyanga na kufariki papo hapo,” alisema Ng’ang’a.

Dereva wa lori hilo aina ya Mitsubishi, Peter Macharia, wa umri wa miaka 46, alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Subukia, ambapo maafisa wa polisi walifika haraka pahala pa tukio.

“Maafisa wa polisi waliupelekwa mwili wa mwendazake katika ufuo wa hospitali ya kaunti ndogo ya Nyahururu na utafanyiwa upasuaji ili kubaini chanzo cha kifo chake,” aliongeza.

Lori hilo limezuiliwa katika kituo cha polisi cha Subukia.