Share news tips with us here at Hivisasa

Eunice Oliala kutoka muungano wa walio na ulemavu wa macho amesema kuwa dawa za kulevya ni miogoni mwa mambo ambayo yamehusishwa na ongezeko la dhuluma za kijinsia.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake walio na ulemavu, kaunti ya Nakuru katika hafla ya kutamatisha kampeni ya siku 16 ya kukabiliana na dhulma za kijinsia, Bi Oliala ambaye ana ulemavu wa macho alisema utumizi wa dawa hizo za kulevya huadhiri jinsi ambavyo watu hufikiria, hatua ambayo huwatatiza katika kusuluhisha matatizo yao ya kila siku.

"Dhuluma za kijinsia huadhiri watu pakubwa kwenye Jamii.  Mojawapo ya sababu zinazosababisha ongezeko la dhulma za kijinsia ni utumizi wa dawa za kulevya.Wale ambao hutumia dawa hizo huadhirika haswa katika kutekeleza maswala mbalimbali na pia hutatizika katika kutatua shida zinazowakumba kila siku," aliashiria Oliala.

Oliala aliendelea kusema kuwa sababu zingine zinazosababisha ongezeko la dhuluma za kijinsia ni ongezeko la gharama ya maisha, hatua ambayo hufanya maisha kuwa magumu. Ongezeko la gharama ya maisha kwa muujibu wake hufanya wengine kukosa uvumilivu.

Amaeangazia pia swala la utamaduni ambalo amesema huwaadhiri baadhi ya watu pale ambapo wanahisi kuwa wenye nguvu zaidi kuliko wachumba wao, huku wengine wakihisi kana kwamba wana haki ya kufanya chochote watakacho.

"Ongezeko la gharama huwaadhiri wengi na kufanya maisha yao kuwa magumu. Baadhi ya watu pia hutaka mambo yafanywe wanavyotaka isitoshe, tamaduni pia huwaadhiri wengine ambao huona kana kwamba wanaruhusiwa kuwadhulumu wenzao," alisema Oliala.