Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amewaonya wanaoendesha baishara ya maji mjini humo kinyume cha sheria kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi kabla ya kuelekea Malindi, Joho alisema kuwa serikali ya kaunti itaanzisha msako katika siku za hivi karibuni kubaini na kuwatia nguvuni watu waliounganishiwa maji kimagendo na kisha baadaye kutumia fursa hiyo kuhitilafiana na usambazaji wa maji kwa wakaazi.

“Ikiwa una maji katika banda lako na hukuunganishiwa na kampuni ya maji ya Mombasa (Mombasa Water Company), basi ujue serikali ya kaunti inakukujia. Hatuwezi kubali wachache waumize wengi wanaofuata sheria,” alisema Joho.

Kulingana na wakaazi mjini humo, wenye mabanda ya maji wanaohudumu kinyume cha sheria husababisha maji kupotea kila mara na kisha baadaye kuwauzia maji hayo kati ya shilingi 50 na 70 kwa mtungi mmoja.

Mapema mwaka huu, Kaunti za Mkoa wa Pwani hususan Mombasa zilikumbwa na tatizo la maji baada ya kampuni za kusambaza maji kusitisha huduma zake kwa madai ya malimbikizi ya madeni.