Idara ya usalama eneo la Kisauni imesema itaanzisha uchunguzi wa vibanda vya mchezo wa pool.
Hatua hii inanuia kuwanasa vijana wadogo ambao hutoroka shule na badala yake kutumia muda wao kucheza mchezo huo pasi na kujihusisha na mambo muhimu maishani.
Idara hiyo ikiongozwa na naibu OCPD wa Kisauni Walter Abondo, imesema idadi kubwa ya vibanda vya pool katika eneo hilo vimekuwa maficho ya vijana wengi wanaokwepa masomo.
Abondo amesema kuwa jambo hilo limechangia kwa ongezeko la visa vya utovu wa usalama.
Kwenye mahojiano ya moja kwa moja na mwandishi huyu, Abondo amesema kuwa kuna baadhi ya vibanda vinavyokiuka sheria zilizowekwa na serikali.
Alisema kuna abanda yanayotoa huduma za michezo hiyo mchana na usiku kutwa huku wanaokwenda kucheza michezo hiyo wakitumia vileo vikali pamoja na miraa, hatua ambayo ameitaja kama janga kwa vijana wadogo.
Abondo alisema kuwa vijana wameanza kujiingiza kwenye uraibu huo ambao umewafanya wengi wao kuacha masomo na kuishia kurandaranda mchana na usiku katika sehemu mbalimbali za eneo hilo.
“Japo kuna vibanda vilivyo na stakabadhi, bado kuna vile ambavyo vinaendesha kazi hiyo kinyume cha sheria. Vibanda hivyo ndivyo vinavyoaminika kuwaficha vijana wadogo ambao mwishowe huishia kutumia mihadarati na kisha baadae kujiunga na makundi ya kihuni,” alisema Abondo.
OCPD huyo alisema kuwa maafisa wa usalama wanaoshika doria eneo hilo sasa wametwika jukumu la kuchunguza vibanda vyote vikiwemo vile vilivyo na leseni.
Aidha, amewaomba wazee wa mitaa kushirikiana na maafisa wa polisi ili kukomesha tabia hiyo ambayo ameitaja kama janga kwa wengi wa vijana wa Kisauni.