Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mahakama ya Mombasa imeagiza vijana 17 waliokamatwa katika maeneo ya Buxton na Tononoka kuzuiliwa kwa siku tano.

Hii ni baada ya afisa mpelelezi Safari Chea, kuwasilisha ombi mbele ya mahakama siku ya Jumatatu, ya kutaka kupewa muda zaidi ili kumwezesha kuwapa wakaazi fursa ya kubaini iwapo vijana hao ndio wamekuwa wakihusika na visa vya uhalifu katika maeneo hayo.

Aidha, alisema kuwa muda huo pia utawawezesha waliothirika kuandikisha ripoti na kuandaa fomu za P3.

Chea alieleza mahakama kuwa vijana hao wanadaiwa kuhusika na visa vya uhalifu kama vile wizi wa kimabavu.

Vijana hao walikamatwa usiku wa kuamkia siku ya Jumapili wakiwa wamejihami kwa panga na visu.

Hakimu Irene Ruguru aliagiza washukiwa hao kuzuiliwa katika Kituo cha polisi cha Makupa hadi siku ya Ijumaa watakaposomewa mashtaka yanayowakabili.