Wanawake 16 na wanaume 14 wamekamatwa na maafisa wa polisi eneo la Likoni, katika oparesheni maalum iliyolenga makahaba wanaofanya kazi katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa OCPD wa Likoni Willy Simba, maafisa wa polisi wanafanya uchunguzi kubaini iwapo kuna vijana walio chini ya miaka 18 miongoni mwa waliokamatwa katika oparesheni hiyo ya Alhamisi.
Hatua hiyo ilichukuliwa kufwatia vilio kutoka kwa wakaazi wanaoshi katika maeneo ya Likoni, waliolalamikia ongezeko la makahaba, huku wengine wakiwa na umri mdogo.
Aidha, baadhi ya wakaazi wamekashifu jinsi biashara hiyo inavyoendeshwa, kwaani baadhi ya makahaba hao huhudumu hata wakati wa mchana, hali ambayo inahofiwa kuathiri maadili ya watoto.
Baadhi ya wafanyabishara ikiwemo wauzaji wa chakula wanaohudumu karibu na kivuko cha feri cha Likoni walilazimika kufunga biashara zao mapema wakihofia kukamatwa licha ya kutokua na makosa.
Haya yanajiri baada ya Kamishna wa Mombasa Maalim Mohamed pamoja na Mbunge wa Mvita Abduswamad Sharrif Nassir, kuwapa wazazi makataa ya wiki moja kuhakikisha kuwa wanao walioacha shule wamerudi shuleni, la sivyo wakabiliwe na mkono wa sheria.