Maafisa wa usalama Kaunti ya Mombasa wanawazuilia vijana 41 katika eneo la Shanzu kwa tuhuma za kupanga njama ya kuvuruga uchaguzi mkuu ujao.
Akithibitisha kisa hicho, mshirikishi mkuu wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa alisema kuwa vijana hao walikamatwa siku ya Jumatano usiku.
Marwa alisema kuwa vijana hao ambao wanatoka kaunti tofauti nchini, walikuwa wamekodishiwa nyumba moja katika eneo la Shanzu.
Akiwahutubia wanahabari mjini Mombasa, Marwa alisema kuwa walipata taarifa hiyo kutoka kwa umma.
Alisema kuwa wakaazi wa eneo hilo waliingiwa na hofu baada ya kugundua kuwa vijana hao walikuwa hawatoki nje wala kuwasha taa nyakati za usiku.
Mshirikishi huyo alisema kuwa vijana hao wanaendelea kuhojiwa na maafisa wa polisi.
Marwa amewataka vijana kutokubali kutumiwa kwa njia yeyote na viongozi kuvuruga usalama hasa wakati huu ambapo taifa linajiandaa kwa uchaguzi mkuu.