Vijana mjini Awasi, Kaunti ya Kisumu wamehimizwa kuunda vikundi kadhaa vya vijana ili kuweza kufaidika na fedha za Serika za miradi kwa vijana za Uwezo Fund.
Kauli hiyo imetolewa na mwanasiasa, Caleb Jakinda ambaye anapania kuwania kiti cha Wadi ya Angoro iliyoko eneo hilo la Awasi ifikapo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Vijana hao ambao wamekua wakilaumu Serikali ya Kaunti kuwaacha nje wakati wa usambazaji wa fedha za maendeleo ya vijana maarufu, Uwezo Fund wametakiwa kuanzisha au kujiunga na vikundi vingine vilivyoundwa tayari ili kufaidika na pesa za miradi kwa vijana.
“Hamwezi kuendelea kuilaumu Serikali kukosa kuwafikia ilhali nyinyi wenyewe ndio hamna muungano wowote. Serikali itawafikia tu iwapo mtajiunga kwa makundi,” alisema Jakinda ambaye alikutana na vijana wanaoendesha kazi za jua kali mjini Awasi mnamo siku ya Ijumaa.
Mwanasiasa huyo aliitetea Serikali ya Kaunti ya Kisumu akisema kwamba imejaribu sana kuwasaidi vijana katika eneo hilo wakati huu wa msimu wa utawala wa ugatuzi, kwamba vijana waliojiunga katika vikundi wamepata fedha za hazina ya maendeleo ya vijana ya Uwezo Fund.
“Niko na ushahidi wa kutosha kwamba baadhi ya maeneo ya Uwakilishi wa Kaunti hii kuna makundi ya vijana ambayo yanaendelea na miradi baada ya kupata pesa za Uwezo,” alihoji Jakinda.
Aidha Jakinda ameomba afisi za Kaunti ya Kisumu zinazosimamia hazina hiyo kurahisisha kazi kwa kuajibikia vikamilifu sheria zilizowekwa wakati wananchi wanapohitaji kutumikiwa ili yeyote asiachwe nyuma na maendeleo ya Serikali kwa uma.