Mwakilishi wa Wadi ya Frere Town Amir Thoya amewahimiza vijana kuungana na kubuni makundi mbalimbali ili kuleta maendeleo katika wadi hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Thoya alisema kuwa vijana wengi mtaani huishia kuwa waraibu wa dawa za kulevya kutokana na kutojihusisha na kazi yoyote, huku akiwanyoshea kidole cha lawama vijana wanaowapora wakaazi wa eneo hilo.

Akizungumza baada ya mkutano wa vijana siku ya Jumamosi, Thoya alisema kuwa japo serikali inajitahidi kubuni nafasi za kazi nchini, ni bora zaidi kwa vijana kuanza kuwa wabunifu na kuanza biashara zao wenyewe ili kuondoa kasumba ya kuhusishwa pakubwa na visa vya uhalifu katika eneo hilo.

Akitoa mfano wa kundi la vijana wa Mkwehu Car wash, Thoya alisema vijana hao ambao huosha magari, pikipiki na hata tuktuk wameendelea kufaidika kwani kwa sasa wanapania kufungua kinyozi.

Ibrahim, mmoja wa vijana wa Mkwehu Car Wash, alisema kuwa kundi lao lilikopa fedha kutoka kwa hazina ya fedha za maendeleo ya vijana al maarufu Youth Fund, na kuanza mradi huo ambao kwa sasa umenawiri kiasi cha kuwawezesha kujikimu kimaisha.

Eneo la Frere Town ni baadhi ya mitaa mjini Mombasa inayokumbwa na visa vya uhalifu, huku vijana wakiishia kuwa wahusika wakuu kutokana na ukosefu wa ajira.