Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya vijana kutoka Kibera wameamua kujionesha kama mfano ulio bora kwa jamii kwa kuanzisha vituo vya kujiajiri ili kupata pesa na mahitaji yao.

Vijana hao wameweka kituo chao karibu na kituo cha D.C mtaani kibera.

Vijana hao wa Junction self help group wameanzisha miradi ya kupanda vyakula, kufuga kuku, sungura na samaki.

Kulingana na mkurugenzi wao Edmonton Mugita, kituo hicho kimewasaidia vijana hao kupata hela ambazo hawangeweza kupata kitambo.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne, Mugita alisema kwamba wameweza kufaidika sana kutokana na mradi wa kufuga samaki.

“Wateja wetu hupenda samaki na wengi wao hutoka katika makazi ya Ubalozi wa Ufaransa,” alisema Mugita.

Alisema kuwa kuku wanaowafuga hununuliwa na wamiliki wa hoteli huko Kibera, ambao huandalia wateja wao kitoweo hicho kila siku ya juma.

Kulingana na Mugita, mradi huo ulioanzishwa 2010 umewawezesha vijana kukusanya pesa ambazo wanatuma nyumbani ili wazazi wao waweze kupata chakula.

Douglas Mosoti, ambaye alijiunga na kundi hilo la vijana 12 mwanzoni mwa mwaka huu, alisema kwamba amefurahishwa na kazi yake ya kupanda mboga.

“Mboga hii hupendwa na watu wengi. Niko na wateja wengi sana na natumai wataendelea kuja kununua. Mradi huu umeniwezesha kununua pikipiki ambayo nimeajiri mtu kuendesha huko mashambani Kisii.

Mosoti amewataka vijana wengine kuanzisha makundi ya kujiajiri ili wapate pesa za kujimudu.