Vijana katika eneo bunge la Kisauni na Kaunti ya Mombasa kwa jumla wametakiwa kujiepusha na viongozi wasiojali maslahi yao.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubia wakaazi katika eneo la Mtopanga huko Kisauni mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mfanyibiashara kutoka Kisauni, Ali Mbogo, alisema kuwa ni jukumu la kila kijana kufikiria maswala muhimu ya kujenga eneo hilo katika siku za usoni.

Mbogo ambaye pia ni mgombea wa kiti cha ubunge cha Kisauni alisema kuwa vijana ndio wenye kulijenga eneo hilo na taifa zima kwa jumla, katika maswala ya maendeleo, usalama, utalii na ujenzi wa miundo msingi.

Mbogo alisema kuwa iwapo vijana watakubali kutumiwa na viongozi wabinafsi basi maswala mengi humu nchini hayatatekelezwa.

Mfanyibiashara huyo alisema kuwa kutokana na kasumba ya baadhi ya viongozi kuwatumia vibaya vijana mashinani katika maswala yao binafsi, viongozi waadilifu wanaofaa kuchaguliwa na vijana kwa minajili ya kuleta demokrasia nchini wanakosa nafasi hiyo.

“Kuna umuhimu wa vijana kujiepusha na viongozi walio na malengo potovu ya kuharibu usalama na maendeleo ya eneo bunge la Kisauni na taifa letu kwa jumla,” alisema Mbogo.

Mfanyibiashara huyo aliahidi kuzuru mashinani na kuwaelimisha vijana na jamii kwa jumla kuhusu jinsi ya kujitenga na viongozi kama hao, hasa wakati huu ambao taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao.