Hali ya taharuki ilikumba eneo la Kisauni siku ya Alhamisi baada ya makundi ya vijana kuandamana na kuziba barabara inayotoka Kengeleni hadi Bamburi, wakilalamikia kuhangaishwa na maafisa wa usalama.
Makundi hayo ya vijana yamesema kwamba tangu maafisa wa polisi wazindue oparesheni ya kiusalama dhidi ya makundi ya kihalifu ya Wakali Kwanza na Wakali Wao katika eneo hilo la Kisauni, wamekuwa wakiwalenga vijana wote hata wale wasiyokuwa na hatia.
Aidha, vijana hao walilamikia tabia ya maafisa wa usalama ambao huingia kwenye majumba yao nyakati za usiku na kuwatia nguvuni wakiwahusisha na maswala ya uhalifu.
Maandamano hayo yalitatiza shughuli za uchukuzi huku matatu zikisitisha safari zao na kuzunguka kupitia barabara ya Bombolulu-Mtamboni na Bamburi.
"Hatuta nyamaza kimya bali tutaendelea kulalamikia hali hiyo hadi pale maafisa wa usalama watakapowatia nguvuni wahalifu na wala sio vijana wasiyokuwa na hatia,” alisema Hussein Ali, mmoja wa vijana hao.
Hatahivyo, naibu Afisa Mkuu wa Polisi katika eneo la Kisauni Walter Abondo, alikanusha madai hayo na kusema kwamba maafisa wa usalama wamekuwa wakiwasaka wanachama wa makundi ya kihalifu ya Wakali Kwanza na Wakali Wao, wala hawajaingia kwenye nyumba za makaazi kwa lengo la kuwahangaisha wakaazi.
Aidha, aliwataka vijana hao kuwasilisha lalama zao rasmi kwa wakuu wa polisi katika Kaunti ya Mombasa iwapo wanahisi kudhulumiwa.