Vijana katika Kaunti ya Kisii wamehimizwa kutumia taaluma zao kujiendeleza kimaisha na kujenga uchumi wa taifa.
Ushauri huo umetolewa baada ya kubainika kuwa, ikiwa uchumi wa taifa unahitaji kupanda zaidi, sharti vijana washiriki kikamilifu katika kujenga nchi ya Kenya kiuchumi.
Akizungumza siku ya Jumapili katika eneo la Etago, mwenyekiti wa chama cha maskauti katika kaunti ya Kisii Caleb Ondieki, aliwataka vijana katika kaunti hiyo kujianzishia kazi kutokana na taaluma zao ili kumaliza umasikini katika jamii na kuchangia kuinua uchumi wa kaunti ya Kisii na kwa taifa la Kenya badala ya kutegemea kazi za uajiri.
Aidha, Ondieki alisema kuna haja vijana kuonyesha nia ya kujiendeleza kwa kuwajibika vikamilifu kwa kushiriki katika ujenzi wa uchumi kupitia utumizi wa taranta zao pamoja na taaruma zao.
''sisi vijana wakati wetu umewadia ambapo tunastahili kuamka na kuchangia vikamilifu katika maendeleo ya taifa letu kwa kufanya kazi kutokana na taaluma zetu,'' alisema Caleb Ondieki.
Wakati huo huo, Ondieki alisema kuwa idadi nyingi ya vijana katika kaunti ya Kisii wamesomea taaluma mbalimbali na hivyo basi hawanabudi kutumia taaluma hizo kujiendeleza kimaisha na kuinua uchumi.
Pia aliwashauri vijana kujiandikisha kwa vikundi mbalimbali ili kukabidhiwa pesa na serikali kuu pamoja na zile za kaunti ili kuwapiga jeki kwenye miradi yao kupitia mradi wa hazina ya maendeleo ya vijana ya Uwezo Fund na kufanya mengi.