Baadhi ya vijana kutoka eneo bunge la Kitutu Masaba wameitaka kamati ya hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge CDF, kuwahusisha kwenye makadirio ya bajeti.
Wakiongozwa na kiongozi wa vijana katika eneo hilo Calvin Osiemo, vijana hao walisema kuwa hawajui sababu ya kamati hiyo kutowahusisha kwenye mipango yake.
Osiemo alisema kuwa kamati hiyo iliwatenga pakubwa kwenye makadirio na mipango yake mwaka jana.
“Ombi letu kwa kamati ya CDF katika eneo hili ni kutuhusisha kwenye kamati za makadirio ya bajeti kwa kuwa tumegundua kuwa kuna miradi ambayo haijakuwa ikitekelezwa hata baada yakutengewa fedha," alisema Osiemo.
Osiemo aidha alihoji kuwa pesa zilizotengewa masuala ya spoti kwenye bunge hilo kwenye mwaka wa bajeti 2014-2015 hazikutumika kwa kuwa hakukuwa na michezo ya aina yeyote iliyofanywa katika eneo bunge hilo.
Alisema kuwa wakaazi wa eneo hilo wanastahili kuchunguza hali hiyo.
"Sheria za taifa hili zinaturuhusu kufahamu jinsi pesa zinazotengewa miradi ya umma zinavyotumika, na ndio maana ninawahimiza wakaazi wa eneo hili kujitokeza kuchunguza jinsi pesa za umma zinavyotumika," aliongezea Osiemo.