Vijana kutoka eneo bunge la Likoni, Kaunti ya Mombasa, wametakiwa kuchukua nafasi ilioko kwa sasa kuwania viti vya kisiasa kama njia moja ya kufanya mabadiliko kwenye jamii.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumanne, mwasiasa mmoja ambaye anamipango ya kuwania kiti cha ubunge cha eneo la Likoni, alisema kuwa hatua hiyo itaondoa dhana kuwa uongozi umehifadhiwa wazee pekee.
Rama Mwalim alisema kuwa vijana ndio uso wa nchi ya Kenya na ni vyema zaidi kuanza miradi au kujifahamisha kwenye wapiga kura kwa kuuza sera zao kwa kuwa kuna chini ya miezi kumi na minane kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2017.
Mwanasiasa huyo alitoa onyo kwa wanasiasa wakongwe kwa kusema kuwa chuma chao kiko motoni kwa kuwa ni wakati wa vijana kukoma kutumiwa na wanasiasa amabao hukosa kuwatimizia mahitaji pamoja na ahadi wanazozitoa nyakati za kufanya kampeni.
Aidha, aliwasihi vijana kuepuka kutumia ghasia wanapojihusisha na masuala yoyote ya kisiasa, na kuwaomba kuwa waangalifu na kuwapiga darubini baadhi ya viongozi ambao mara nyingi huwatumia kuzua ghasia kwa manufaa yao ya kibinafsi.
“Viongozi wakuu huwa hawataki kushindwa na hutumia mkato kwa kuwalipa vijana ambao hawana kazi pesa kidogo, ili kuwatia hofu wapinzani wao,” alisema Mwalim.
Kwa sasa wanasiasa kutoka eneo hilo la Likoni wameonekana wakitembea mitaani kama njia moja ya kuwashawishi wakaazi ili kuwapigia kura ifikapo mwaka wa 2017.