Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mombasa amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asili mia 75 ya vijana katika eneo la Pwani wamekosa kujiunga na vyuo vikuu kutokana na ukosefu wa karo.
Mahmoud Salim amesema kuwa hali hiyo inaweza kukabiliwa iwapo serikali kuu na zile za kaunti zitashirikiana kujenga taasisi mbalimbali za kiufundi ili kuwawezesha vijana waliokosa nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu wanapata mafunzo ya kiufundi.
Katika mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumanne, afisa huyo tawala alisema kuwa tayari zoezi la kukusanya majina ya vijana wasio na ajira mitaani pamoja na wale waliokosa kujiunga na vyuo vikuu limeanzishwa ili kupata idadi kamili ya vijana watakao saidiwa kupata ajira.
"Tunapanga mikakati ya kuhakikisha kuwa vijana wote waliomaliza shule na hawajafaulu kujiunga na vyuo vikuu wanatafutiwa nafasi za ajira ili kuzuia uhalifu,” alisema Salim.
Akigusia swala la usalama katika Kaunti ya Mombasa, Salim alisema kuwa idara ya usalama itahakikisha kuwa makundi yote ya kihalifu katika kaunti hiyo yameangamizwa, huku akiwataka wakaazi kushirikiana na maafisa wa polisi kutoa habari kuhusu washukiwa wa uhalifu.