Vijana mjini Mombasa wamelalamika kuwa maafisa wa polisi wanawalenga wanapotekeleza opereshani zao za kukabili visa vya uhalifu mjini humo.
Wakiongozwa na viongozi wao, vijana hao walidai kuwa maafisa wa usalama huwahangaisha na hata kuwatia mbarani vijana wasiokuwa na hatia, na kisha baadaye kuwasingizia kuwa wanajihusisha na visa vya utovu wa usalama.
Mmoja viongozi wa vijana hao Abubakar Swabir, amedai kuwa maafisa wa polisi hutumia nguvu kupita kiasi wanaposaka washukiwa wa ugaidi mjini Mombasa.
“Kila mmoja anataka usalama wa kutosha lakini isiwe kutoa usalama kunageuka kuwa mateso kwa watu wasio na makosa. Vijana wengi sasa wanaogopa hata kutembea barabarani kwa hofu ya kuhangaishwa na polisi,” alisema Swabir.
Kiongozi huyo alisema kuwa baadhi ya familia za waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika na ugaidi hupitia mateso mbalimbali mikononi mwa maafisa wa polisi, kwa madai kuwa wanataarifa zaidi kuhusu ugaidi.
Vijana hao sasa wanaitaka idara ya usalama kuwa na utu katika harakati zao za kutoa ulinzi kwa wenyeji.