Vijana katika kaunti ya Mombasa na ukanda wa Pwani kwa jumla wametakiwa kujiepusha na utumizi wa miraa hasa wanapokuwa katika shughli zao za kikazi.
Akiongea na mwanahabari huyu afisini mwake mjini Mombasa siku ya Ijumaa, mwakilishi wadi mteule katika bunge la Kaunti ya Mombasa, Fatma Kushe, alisema kuwa vijana wengi hasa madereva wa magari, wanamazoea ya kutumia miraa wanapokuwa kazini.
Kiongozi huyo aidha aliwaonya madereva hao wa magari ya umma dhidi ya kutumia miraa wakati wanapokuwa kazini ili kuepukana na utovu wa nidhamu barabarani.
“Tunataka vijana wetu kujiepusha na utumizi wa miraa kwani huwasababishia madhara makubwa hasa hawa madereva wa magari. Iwapo basi watazingatia hilo, watajiepusha na maovu mengi,” alisema Kushe.
Alisema kuwa iwapo wana haja ya kutumia miraa, basi ni bora kufanya hivyo wakati wa mapumziko.