Vijana katika Kaunti ya Mombasa wametakiwa kujitenga na vishawishi vinavyowasukuma katika kushiriki uhalifu na kujiunga na ugaidi, ili kaunti iwe salama.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano katika kongamano la kuhamasisha vijana, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki alisema kuwa vijana wana jukumu kubwa katika kudumisha usalama, kwani wana ufahamu wa mambo mengi yanayoendelea katika mitaa yao.
Achoki aliwataka vijana kuhakikisha kuwa wanashirikiana na maafisa wa polisi katika juhudi za kudumisha amani sambamba na kutaja washukiwa wa uhalifu ili watiwe nguvuni.
Kamishna huyo alisema kuwa idara ya usalama ina mpango wa kuhakikisha kuwa vijana hawajiunga na uhalifu na badala yake wanashiriki katika maswala ya kujiendeleza kimaendeleo kwa kutumia miradi ya serikali kuu na ile ya kauti.
“Tunawaomba vijana kujitenga na vishawishi vibaya na kujishughulisha na maswala ya maendeleo ili Kaunti ya Mombasa iwe salama,” alisema Achoki.
Alitaja usalama kama jambo muhimu katika kuimarisha nchi, na kuongeza kuwa kuwepo kwa amani kutapelekea watalii zaidi kuzuru Kaunti ya Mombasa.