Vijana katika Kaunti ya Mombasa wamehimizwa kujitenga na viongozi wabinafsi wasiojali maslahi yao, licha ya kuwataka vijana hao kuwachagua wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Afisa wa Haki na Sheria katika shirika la kutetea haki za kibinadamu nchini la Haki Afrika, Francis Gamba, amesema kuwa vijana wanafaa kujitenga na viongozi kama hao ili kujiepusha na msukumo wa kisiasa na kujihusisha na uhalifu.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne katika mkutano wa hamasa, Gamba alisema kuwa ili vijana kuwa na amani na kuzidi kuchangia katika maswala mbalimbali ya kimaendeleo, lazima wajiepusha na viongozi wasiojali masalahi ya vijana na kutaka kuwatumia kwa manufaa yao binafsi.
"Tafadhali vijana hakikisheni mnajiepusha na viongozi kama hawa na kujiunga na makundi ya vijana kuteleleza maswala muhimu ya kimaendeleo, sambamba na kuhubiri amani ili kuhakikisha Wakenya wanaishi kwa amani,” alisema Gamba.
Kauli ya mwanaharakati huyo inajiri huku baadhi ya viongozi wa kisiasa wakionekana kuwashauri vijana kuwa wafuasi wao na kuzua vurugu katika maeneo mbalimbali.