Vijana katika Kaunti ya Mombasa wametakiwa kukumbatia kilimo.
Wajumbe kutoka Idara ya kilimo Kaunti ya Mombasa wamesema kuwa vijana wanafaa kubadili mawazo yao ya namna wanavyotafta mapato.
Wajumbe hao walisema kuwa kilimo ndicho huchangia pakubwa kwenye uchumi wa taifa.
Wakizungumza na vijana katika Hoteli ya Panorama mjini Mombasa, wajumbe hao walisema iwapo vijana wa Mombasa watakumbatia kilimo, basi huenda wengi wao wakabadili mienendo yao, kwani biashara hiyo itawawezesha kujikimu kimaisha.
Kulingana na kaimu mkuu wa idara ya kilimo Kaunti ya Mombasa Anthony Njaramba, serikali ya kaunti itajitolea kuwasaidi vijana watakao buni makundi na kuanzisha miradi ya kilimo.
“Idara yangu itaandaa warsha maalumu ili kuwapa vijana mafunzo ya jinsi ya kupanda na kukuza mimea ya mboga kama vile nyanya, sukuma wiki, pilipili, miongoni mwa mazao mengine yanayotumika kama mboga kwa binadamu,” alisema Njaramba.
Aidha, alisema kuwa ikiwa vijana watashirikiana vilivyo, basi huenda Kaunti ya Mombasa ikawa ya kwanza kwa vijana kubuni nafasi za kazi kwa wenzao.
Aidha, alisema kuwa hiyo ni njia mojawapo ya juhudi za serikali ya Kaunti ya Mombasa za kutafuta suluhu kwa ukosefu wa ajira.