Vijana katika kaunti ya Mombasa wameonywa kujitenga na utumizi wa mihadarati na badala yake kujihusisha na maswala ya kuimarisha maisha yao.
Afisa wa Haki na Sheria katika Shirika la kutetea haki za kibinadamu nchini Haki Afrika, Francis Auma amesema kuwa japo idadi kubwa ya vijana wameanza kujitenga na maswala hayo lakini kuna umuhimu wa kuwashawishi vijana hao kujitenga na mihadarati.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Auma amesema kuwa hatua ya vijana kujiunga na utumizi wa mihadarati na uhalifu katika kaunti ya Mombasa na eneo zima la Pwani imechangia na ukosefu wa ajira na msingi bora wa maisha kutoka kwa jamii.
Aidha, amewataka vijana kubuni makundi ya maendeleo ili kufaidika na miradi mbalimbali inayotolewa na serikali kuu na zile za kaunti ili kujikimu kimaisha.
"Tunawaomba vijana kuhakikisha wanajitenga na maswala ya mihadarati na kujihusisha na mambo ya maendeleo ili wafaidike na miradi inayotolewa na serikali",alisema Auma.
Mwanaharakati huyo wa kijamii imeahidi kuwahasisha vijana kufahamu athiri za utumizi wa mihadarati na uhalifu na badala yake kujihusha na maswala muhimu ya maendeleo.