Vijana katika kaunti ya Mombasa wametakiwa kujiepusha na viongozi wenye malengo binafsi na wasiojali maslahi ya vijana.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumanne, mwanaharakati wa kisiasa katika eneo la Kisauni Ali Mbogo, alisema kuwa vijana wengi katika eneo la Kisauni na kaunti nzima ya Mombasa wanatumiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa ili kuzua taharuki na kusababisha ukosefu wa usalama.
Mbogo ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu mjini Mombasa, alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuleta upotovu wa maadili miongoni mwa vijana katika eneo hilo.
Aliitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwatafutia vijana mbinu za kujikimu kimaisha.
Aidha, amewataka viongozi wanaopanga kuwatumia vijana kwa manufaa yao ya kibinafsi kukomesha fikira hizo.
Mbogo alisema kuwa fikira kama hizo ndizo zinazochangia kuzuka kwa makundi ya kihalifu ambayo huwahangaisha wakaazi.
"Tunawaomba vijana kuwa makini na viongozi kama hawa wenye kuwadhulumu na kuwalaghai wafanye uhalifu kwa manufaa yao binafsi,” alisema Mbogo.
Kauli ya mwanaharakati huyo inajiri siku chache tu baada ya kuvamiwa na genge la vijana alipokuwa ametoka kwa hafla ya mazishi katika eneo la Kisauni.