Kufuatia ongezeko la mikasa katika eneo bunge la Mvita, Shirika la Msalaba Mwekundu kwa ushirikiano na uongozi wa eneo hilo limezindua mikakati ya kuwafunza vijana mbinu za kukabiliana na majanga.
Katika kikao kilichowajumuisha maafisa wa shirika hilo na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, iliafikiwa kuwa mbunge huyo atafadhili mafunzo kwa vijana wa eneo hilo, ili wapate fursa ya kujifunza mbinu za kuokoa maisha kunapotokea majanga.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika eneo la Mvita, afisa mkuu wa shirika hilo Kaunti ya Mombasa Mohammed Rajab, alisema kuwa hatua hiyo pia itawasaidia vijana kujiepusha na visa vya uhalifu.
"Tumeonelea kuandaa kikao hichi ili kuwasaidia vijana na jamii kwa jumla kufahamu mbinu mbalimbali za kukabiliana na majanga pindi yanapotokea. Tutashirikiana na viongozi wa eneo hilo kufanikisha lengo hilo,” alisema Rajab.
Haya yanajiri baada ya mkasa wa moto kushuhudiwa hivi juzi ambapo mali ya thamani ya maelfu iliharibika baada ya moto kuyateketeza maduka matatu katika mtaa wa Majengo.