Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira, Timothy Bosire amewaomba vijana wa eneo bunge hilo kutotumiwa na wanasiasa kurudisha maendeleo ya eneo hilo nyuma.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Rigoma, mbunge huyo alisema kuna wanasiasa wanawatumia vijana wa eneo hilo ili kukosoa uongonzi wake.
Wanasiasa hao wanadai kuwa hafanyi maendeleo katika eneo hilo jambo ambalo amekerwa nalo na kuomba vijana kushirikiana naye kuinua maendeleo ya eneo hilo.
Hii ni baada ya baadhi ya vijana wa eneo hilo kujitokeza na kuchukua hatua ya kulima barabara za eneo hilo huku wakisema zikarabatiwe haraka.
Bosire aliwahakikishia wakaazi wa eneo hilo kuwa hakuna pesa za kuzikarabati barabara hizo katika hazina na kusema pindi pesa hizo zitaingia kwa hazina ya ustawi maeneo bunge, barabara hizo zitakarabatiwa kikamilifu.
“Nawaomba muwe watulivu. Nitazikarabati barabara zote za eneo hili pindi pesa zitakapoingia kwa hazina ya ustawi maeneo bunge,” alidokeza Timothy Bosire.
Wakati huo huo, mbunge huyo aliwaomba vijana kushirikiana na viongozi waliochaguliwa ili kuhakikisha maendeleo yamefanywa na kutimizwa kikamilivu na kujiimarisha na kujiendeleza kimaisha badala ya kutumiwa na wanasiasa ambao hawana maono ya siku za usoni.
“Wale wanasiasa wanawatumia vijana kurudisha maendeleo nyuma nawaomba muweke siasa kando tufanyie wananchi maendeleo maana tulichagulliwa kutimiza ahadi tulizotoa kwa wananchi,” aliongezea Bosire.