Kamanda mkuu wa Polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi amewaonya vikali vijana wanaojihusisha na utumizi wa mihadarati na uhalifu kukoma mara moja la sivyo maafisa wa usalama watawakabili kikamilifu.
Akitoa onyo hilo mjini Mombasa siku ya Ijumaa katika makao makuu ya idara ya usalama, Wanjohi amesema kuwa idadi kubwa ya vijana mjini Mombasa na eneo zima la Pwani wamejitosa katika utumizi wa mihadarati na uhalifu na akisema kwamba lazima swala hilo kusitishwa.
Amesema kuwa tayari maafisa wa usalama wanaendeleza msako mkali ili kuwatia nguvuni vijana wanaojihusisha na uhalifu na kuwahangaisha wakaazi huku akiwataka vijana hao kuachana na maswala ya uhalifu na kushirikiana na jamii zao vyema.
"Tunawataka vijana kujiepusha na utumizi wa mihadarati na uhalifu la sivyo maafisa wa polisi watawakabili kisheria na pia wajihusishe na mambo ya kuwasaidia katika siku za usoni," alisema Wanjohi.
Zaidi ya vijana 17 kufikia sasa wanaendelea kuzuiliwa baada ya kutiwa nguvuni na maafisa wa polisi kwa kuhusika na uhalifu na kuhangaisha wakaazi Mombasa.