Vijana katika eneo la Pwani wamehimizwa kuwa makini na viongozi wa kisiasa wanaowasukumu kuzua vurugu na kuwatia hofu wakaazi ya kuwepo na ukosefu wa kiusalama.
Kulingana na Afisa wa Haki na Sheria katika Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu Haki Afrika, Francis Auma Gamba, vijana wengi eneo la Pwani wanashawishia na viongozi wa kisiasa kutatiza usalama wa eneo hili.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamsi, Auma amesema kuwa njia pekee ya kutatua maswala ambayo serikali imeonekana kuyaweka kando ni kupitia mazungumza lakini sio viongozi kuwashawishi vijana kutekeleza maovu na kuchangia uhasama miongoni mwa jamii.
Amesema kuwa kwa sasa wameanzisha kampeni ya kuwahamasisha vijana jinsi ya kuepukana na viongozi kama hao na kuhakikisha kuwa wanadumisha amani ili taifa hili liwezekufanikisha ajenda zote za kimaendeleo mashinani.
"Kama shirika tumeanzisha kampeni za kuwahamasisha vijana kujua namna ya kuepukana na viongozi kama hao ili kuona kuwa swala la usalama nchini unaimarisha na uchaguzi mkuu kufanyika kwa amani bila hofu yoyote ambayo tayari imeanza kuwaingia wakaazi",alisema Auma.
Mwanaharakati huyo wa kijamii ameahidi kuwaunganisha vijana pamoja ili kuona kuwa eneo la Pwani liko salama kabla ya uchaguzi mkuu kuwadia.