Vijana katika ukanda wa Pwani wametakiwa kukumbatia elimu na kutia bidii masomoni ili waweze kupata elimu ya juu.
Akizungumza kwenye mkutano na vijana katika Shule ya msingi ya Bonje huko Rabai, mwenyekiti wa chama cha ushirika cha vijana wa eneo hilo, Petronila Sidi, alisema japo vijana wa Pwani wana vipaji, ni sharti watilie maanani umuhimu wa kuongeza viwango vya elimu kwa kujiunga na vyuo mbalimbali.
Sidi alisema kuwa vijana wengi katika eneo la Pwani husalia na viwango vya elimu vya chini kama vile vya diploma na cheti kutokana na uzembe.
Alizipa changamoto serikali za kaunti katika eneo la Pwani kuyapa maswala ya elimu kipaumbele kwa kufadhili masomo ya wanafunzi katika vyuo kikuu na hata shule za upili.
Aidha, amewataka vijana kufanya kazi kwa bidii akiongeza kuwa wana nafasi kubwa ya kuendeleza masomo yao kwa kuwa serikali za kaunti za Pwani zimejitolea kuwasaidia kwa kila namna.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Youth Action Movement tawi la Rabai Anderson Tsuma, amewataka vijana kudumisha amani na uwiano na kukumbatia masomo.
Alisema kuwa masomo ni njia mojawapo ya kuwafanya waweze kuwa na mstakabali mwema katika jamii.
Aidha, Tsuma alisema kuwa endapo vijana watakumbatia umuhimu wa elimu, serikali za kaunti zitawapa zabuni mbalimbali za miradi ya maendeleo, kauli ambayo iliungwa mkono na Petronila Sidi ambaye alisisitiza umuhimu wa vijana kukumbatia elimu ya juu.