Vijana katika ukanda wa Pwani wametakiwa kutumia maarifa waliyoyapata kwenye kozi mbalimbali walizosomea kuanzisha biashara ili waweze kujikimu kimaisha.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza na vijana huko Mariakani, afisa mkuu anayehusika na usimamizi wa fedha za maendeleo ya vijana Lennox Mwabaya, alisema kuwa vijana wengi katika eneo la Pwani wanakaa nyumbani licha ya kuwa na maarifa katika maswala mbalimbali.

Alisema kuwa baadhi ya vijana ni wabunifu wa kuanzisha biashara zao lakini huishia kudharau taasisi walizosomea kwa kuwa hazitambuliki, hivyo basi kuwanyima nafasi ya kupata ajira katika kampuni mbalimbali hapa nchini.

Mwabaya alisema kuwa kuna mengi ambayo vijana wanaweza kujihusisha nayo katika kutafuta riziki ya kila siku na hata kujikimu kimaisha, huku akisema kuwa kwa sasa wanapaswa kuunda makundi na kutumia fedha za serikali kama vikundi vya vijana kujiendeleza kwa kuanzisha biashara.

Mwabaya pia alisema kuwa vijana wengi ambao hawajihusishi na chochote maishani ndio wanaoaminika kuwatunga wanafunzi mimba za mapema, huku akisema kuwa hali hiyo imekithiri sana katika eneo la Pwani.

“Vijana wanafaa kufika kwenye afisi za fedha za maendeleo ya vijana wakiongozwa na wenyekiti wao katika makundi ili waweze kufaidika na fedha za vijana zinazotolewa na serikali,” alisema Mwabaya.

Hatahivyo, vijana waliohudhuria mkutano huo walisema sio kuwa wanapenda kuishi nyumbani bila kufanya kazi wala kujihusisha na biashara, ila ni kwa kukosa kujua namna watakavyopata fedha za hazina ya Uwezo ambazo serikali huwatengea ili kujiendeleza kimaisha.

Miongoni mwa viongozi waliofika kwenye mkutano huo ni pamoja na chifu wa Ruruma Hezron Gumo.