Vijana katika kaunti ya Uasin gishu watafaidika kutokana na vibanda vilivyojengwa na wizira ya biashara ya kaunti ya uasin gishu.
Akizungumza afisini mwake siku ya Jumatano, waziri wa biashara katika kaunti ya Uasin gishu Philip Melly alisema Kuwa asilimia kubwa ya vibanda hivyo vitakodeshewa kwa vijana punde tu vitakapo kamilika.
“Asilimia kubwa itapewa vijana ili waweze kujiendeleza kimaisha,” alisema Melly.
Waziri huyo alisema kuwa vibanda hivyo vitasaidia kupunguza msongamano wa wachuuzi wa rejareja katika kaunti hiyo.
“Vibanda hivi vimetengewa pahali pa teule kwa hivyo vinachukua nafasi ya zile vibanda ambavyo vilibomolewa,” alisema Melly.
Hata hivyo, Melly alizidi kuwahimiza vijana kujiunga na vikundi vya kijamii almaarufu ‘Saccos” ili kuweza kupata ufadhili kwa urahisi.
“Kuna fedha kama vile ‘Youth Enterprice Fund’ ambazo zinaweza kugawanywa kwa urahisi ikiwa vijana watakuwa wamejiunga na makundi mbalimbali,” alisema Melly.
Melly alisema kuwa ujenzi wa vibanda hivyo bado unaendelea katika sehemu mbalimbali ya kaunti na punde tu vitakapomalizika, vitaweza kuimarisha maisha ya wakaazi.