Muungano wa vijana kutoka kaskazini mwa Bonde la Ufa unatishia kwenda mahakamani kupinga hatua ya kusimamishwa kazi kwa mwenyekiti wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) Mumo Matemu na naibu wake Irene Keino.
Chini ya muungano wao wa North Rift Youth Forum, vijana hao wanasema kwamba kumsimamisha kazi mwenyekiti huyo ni njama ya kudidimiza juhudi za kupambana na ufisadi nchini, jambo ambalo wamesema kamwe hawatalikubali.
Vijana hao wamesema kwamba hatua hii itaathiri vita dhidi ya ufisadi nchini, huku wakiongeza kwamba wako tayari kwenda kortini na wanasubiri mawaidha kutoka kwa mawakili wao.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao Hezekiah Kosgei, aidha walisema watatumia mbinu zingine iwapo ombi lao halitakubalika mahakamani.
Kosgei amesema watashinikiza vijana kote nchini ili kuzungumza kwa sauti moja na kukataa ufisadi.
Mwenyekiti huyo aliongezea kuwa hatua ya kusimamishwa kazi kwa makamishina wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini ni dhuluma kwa viongozi ambao walitakiwa kujiondoa ofisini hivi maajuzi kwa tuhuma za ufisadi.
Kusimamisha kazi kwa Matemu na Keino kulithibitishwa na msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu.
Mwenyekiti wa wa kamishina hiyo Mumo Matemu na naibu wake Irene Keino wamesimamishwa kazi huku wakisubiri kuchunguzwa iwapo wamefanya kazi yao kwa njia inayostahili.
Hii ni baada ya bunge la taifa kupendekeza kubuniwa kwa tume ili kuwachunguza wawili hao.