Muungano wa makundi ya vijana kutoka Kaunti ya Nakuru yamelalamika vikali kwa kile wametaja ni ubaguzi dhidi ya vijana wa kaunti hiyo.
Kwenye kikao na wanahabari Alhamisi hii, mwenyekiti wa muungano huo Charles Njihia alitishia kupanga maandamano makubwa ya vijana dhidi ya uongozi wa Kaunti ya Nakuru kwa kuwa na mkutano katika hoteli moja mjini Nakuru Jumamosi iliyopita wakitathmini atakayekuwa kiongozi wa chama kipya cha Jubillee Party.
Njuguna ameongeza kuwa ingawa vijana ndiyo waliyo wengi, wana uwezo pia wa kuweza kuchukua uongozi wa kaunti hiyo, na kuonya baadhi ya viongozi kutoleta migawanyiko kwa misingi ya kikabila.
Ni matamshi yaliyoungwa mkono na rais wa bunge la vijana la kaunti Phillip Ng’ok aliyeunga mkono hatua ya rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto katika azma yao ya kuunganisha wananchi.
Aidha, Esther Mwai, mwakilishi wa vijana katika eneo bunge la Nakuru mashariki anasisitiza kuwa ni sharti vijana wahusishwe kikamilifu katika uongozi wa Kaunti ya Nakuru kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
Matamshi ya vijana hao yanajiri siku kadhaa baada ya aliyekuwa kaimu mwenyekiti wa chama cha TNA Kaunti ya Nakuru Abdul Noor kupinga mikutano ya kisiri ya baadhi ya viongozi wa kaunti hiyo, akisisitiza lazima uchaguzi wa viongozi wa chama cha Jubillee Party ufanyike na kuhusisha watu wote.