Kundi moja la vijana eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, limezindua mpango wa kuandaa mikutano mbalimbali inayowakutanisha wakaazi wa eneo hilo kujadili maswala muhimu ya maendeleo.
Kundi la Sauti ya Vijana Likoni limezindua mpango huo baada ya kutambua kwamba wakaazi wengi wa Likoni hawafahamu haki zao za kimsingi.
Akizungumza na mwandishi huyu wakati wa uzinduzi huo siku ya Jumapili, Salim Ravino, mwanachama wa kundi hilo, alisema kwamba mikutano hiyo pia itatoa fursa kwa viongozi wa eneo hilo kujadiliana na wananchi.
“Hili ndilo kongamano la kwanza ambapo tumeweka mikakati. Kongamano linalofuata tutakuwa tunachagua hoja maalum ambapo tutashirikiana kuijadili na kutafuta suluhu,” alisema Ravino.
Ravino pia aliongeza kwamba watatoa fursa kwa wenye nia ya kugombea nyadhfa mbalimbali za uongozi kuhudhuria na kutambua matatizo yanayowakumba wakaazi wa Likoni ili waweze kutengeza sera zinazofaa.
Kwa upande wake, Bi Mwanamanga Babu, mshirikishi wa kundi hilo aliwaonya viongozi watakaohudhuria dhidi ya kutumia fursa hiyo kujipigia debe, akisisitiza kwamba haitakuwa mikutano ya kisiasa.
“Hapa hatutaki kujua wewe unatoka katika chama gani.Jambo la muhimu ni kujadili mambo yanayowahusu watu wa Likoni ikiwemo elimu na afya, miongoni mwa mambo mengine,” alisema Babu.
Wakati huo huo, vijana hao pia wametoa wito kwa serikali ya Kaunti ya Mombasa kuanzisha miradi mbalimbali katika eneo hilo, huku wakilalamika kwamba serikali hiyo imewatanga, ilhali inaendeleza miradi katika maeneo mengine ya kaunti.
Hatua ya kundi hilo kuzindua mpango wa kujadili maendeleo unaonekana kuleta mwamko mpya katika eneo hilo, huku ikiwa imesalia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu.