Kikundi kinachofagia mji wa Kisii kimeanza kuchimbua mitaro katika mji huo ili maji yaweze kupita wakati mvua inaponyesha.
Hii ni baada ya mvua nyingi inaonyesha kusababisha mitaro kuziba na maji kufurika katika barabara na kusababisha shida kubwa kwa wakaazi.
Akiongea siku ya Jumanne, mhudumu wa afya ya Jamii na mwenyekiti wa Muungano Group, Kepha King’oina alisema walianza shughuli hiyo ili kuhakikisha kuwa mitaro hiyo imechimbuliwa na maji kupita na kutoka kwa barabara .
Mitaro hiyo itachimbwa kando ya barabara ilioko karibu na hospitali ya Rufaa na mafunzo ya Kisii kuelekea soko la Daraja Mbili.
“Tulianzisha kuchimbua mitaro hii ili kutoa maji kwa barabara kwa kuwa maji hayo husumbua watu wanapokuja hospitalini,” alisema Kepha.
Aidha, aliongezea kuwa wakati maji yamekwama ugonjwa wa malaria huongezeka kutokana na mbu ambao husalia kwa maji hayo na kusambaza ugonjwa huo.
Kikundi hicho cha Minto Muungano Youths kilisema kuwa wamejitolea ili kuhakikisha kuwa mji wa kisii na viunga vyake ni msafi kila wakati ili kujikinga kutokana na magonjwa yanayosababishwa na mazingira machafu.
“Tuliamua kufanya usafi katika mji wetu wa kisii ili kuhakikisha kuwa mji wetu ni msafi na mazingira yetu ni masafi kila kujao,” alisema Samson Barongo, mfanyikazi katika kikundi hicho.
Kwingineko, mwenyekiti wa kikundi hicho alisema kuwa vijana wote na mashirika mbalimbali wanastahili kushirikiana ili kuinua viwango vya usafi katika mji huo.