Madereva wanaotumia barabara kuu ya Mombasa-Nairobi wanasema kuwa kuna kundi la vijana ambalo lina tabia ya kuwafungia barabara na kisha kuwatoza pesa kila wanapopitia njia ya pili inayotumika wakati wa msongamano.
Madereva hao wanasema hulazimika kupitia njia hiyo iliyoko karibu na Miritini ambayo wameruhusiwa na trafiki kutumia kila kunapokuwa na msongamano katika barabara kuu.
Akiongea na mwandishi huyu katika kituo cha mabasi cha Mwembe Tayari siku ya Jumanne, dereva mmoja kwa jina Joel Mutuku alisema kuwa vijana hao huchukua fursa hiyo kuwadhulumu madereva.
“Wale vijana ni wavivu na hawana kazi ya kufanya ya kuwaingizia pesa, na hiyo ndio sababu wanatumia mbinu hiyo kupata pesa na ukikataa kuwapa wanaweka mawe barabarani,” alisema Mutuku.
Aidha, madereva hao wameomba serikali kupanua barabara hiyo ambayo ndio yapekee inayounganisha Mombasa na maeneo mengine ya nchi.
Madereva hao wanasema wameripoti visa hivyo kwa polisi wa trafiki bila hatua yoyote kuchukuliwa, huku wakiongeza kuwa tabia hiyo imewaathiri kwa muda mrefu kwani vijana hao wanaongezeka kila siku.