Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana wawili wamehukumiwa kifungo cha miaka minne na mahakama moja ya Nakuru baaada yao kupatikana na hatia ya kuiba bidhaa mbalimbali kutoka kwa duka moja.

Wawili hao, Samwel Mburu, 26, na Charles Mwangi, 24, walihukumiwa siku ya Jumanne na Hakimu Mkuu Maroro Nyaundi, baada yao kukiri kosa hilo.

Washukiwa hao walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuvunja duka moja na kuiba bidhaa mbalimbali kama vile chumvi, kilo moja ya mafuta ya kupikia, pakiti mbili za sigara, kalamu 24 pamoja na sabuni, miongoni mwa bidhaa zingine, zenye thamani ya shilingi 1,200 mnamo Desemba 22, 2015 katika eneo la Kabazi kwenye kaunti ndogo ya Subukia.

Upande wa mashtaka uliarifu mahakama kuwa mlalamishi ambaye ni miliki wa duka hilo, aliripoti tukio hilo katika Kituo cha polisi cha Kirengero kuwa wawili hao walionekana wakiwauzia wanafunzi kalamu hizo pamoja na vifutio.

Wakijitetea, wawili hao waliarifu mahakama kwamba walilenga kutumia bidhaa hizo nyumbani kwao huku wakiitaka mahakama iwaweke chini ya muda wa majaribio.

Wawili hao sasa wana siku kumi na nne kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Wakati huo huo, Mburu na mwangi walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuiba kondoo mwenye thamani ya shilingi elfu sita kutoka kwa James Njuguna na kisha kumchinja nyumbani kwao Njoro mnamo Desemba 18, 2015.

Hata hivyo, wawili hao walikanusha mashtaka hayo na sasa kesi dhidi yao itasikizwa Januari 18, 2016.