Wamiliki na madereva wa magari katika eneo la Kisauni wamelalamikia wizi wa vipuri vya magari yao kila wanapoyaegesha magari hayo wakisema kuwa umeongezeka kiasi cha kuwatishia.
Samuel Chiro dereva wa gari aina ya matatu katika barabara ya Kisauni kuelekea katikati mwa mji anasema sasa inawalazimu kuwa waangalifu zaidi kila wanapoegesha magari yao kwani vijana wenye umri wa makamo huishia kung’oa sehemu za magari kama vile vio huku wakifungua hata taa za magari ili kwenda kuuza kwenye gereji.
Chiro amesema kuwa vijana hao hutekeleza uhalifu huo kwa haraka pasi kuwatambua na hata wanapojulikana hutoroka upesi na kukimbia jambo ambalo amelitaja kama kuwaharibia kazi kwani kila jioni wanatakikana kufikisha kiasi fulani cha pesa walichoafikiana na wamiliki wa magari huku gari likitakikana kuwa na sehemu zote jambo ambalo huwa ni kinaya kikubwa kwa wengi wa madereva.
Kisa cha hivi punde ambapo vijana wawili walipatikana mchana mweupe wakitekeleza uhalifu huo karibu na kituo cha matatu cha Barsheba huko Kisauni waliiiacha gari moja aina ya texi bila taa za mbele zinazotumika sanasana kuelekeza ama kuonyesha mwelekeo almaarufu Indicators baada ya vijana hao kuzipora taa hizo pasi kujali sheria wala kuogopa mwenye gari hilo.
Kulingana na mumiliki wa texi hiyo Iddi Mohamed anasema muda mchache tu baada ya kuegesha gari lake na kuingia kwenye mkahawa ulioko karibu na barabara alishtuka kuona gari lake halina taa hizo huku walioshuhudia kisa hicho wakikosa kuwachukulia hatua zozote vijana hayo kwa uhalifu waliotekeleza.
Mohamed amesema kuwa kama kwa sasa vijana hao wameanza uhalifu wa jinsi hiyo basi eneo la kisauni huenda likawa tishio kwa wenyeji huku akisema huenda vijana waliokuwa wakitekeleza wizi wa mabavu kwa kuwatishia wenyeji kwa mapanga na hata visu wakawa wameanza mbinu mpya za kuendeleza uhalifu eneo hilo.
Madereva hao aidha wametoa wito kwa idara ya usalama kaunti ya Mombasa kuimarisha usalama eneo hilo kwani kila uchao idadi ya magari yanayoporwa vipuri inaongezeka.