Baadhi ya vijana kutoka kaunti ya Nyamira wamelalamikia pakubwa hatua ya wabunge wa kaunti hiyo kutowashughulikia kuhakikisha wananufaika kutokana na mpango wa kazi kwa vijana.
Kwenye mahojiano na huyu mwanahabari siku ya Jumanne, kiongozi wa shirikisho la vijana kwenye kaunti ya Nyamira, Duke Onyagi alishangazwa na sababu ya mpango huo kutoanzishwa ikizingatiwa kwamba idadi kubwa ya vijana hawana ajira.
“Ni Jambo la kushangaza kwamba miradi ya shirika la huduma kwa vijana NYS haijawanufaisha vijana wengi wa kaunti hii ikizingatiwa kwamba vijana wengi hawana ajira,” alisema Onyagi.
Onyagi aidha aliitaka serikali ya kitaifa kuchukua jukumu la kuhakikisha mpango huo unazinduliwa Nyamira ili kusaidia kupunguza visa vya uhalifu miongoni mwa vijana.
“Ombi langu kwa serikali kuu ni kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa miradi ya shirika hili imeanzishwa hapa Nyamira ili kusaidia katika kupunguza visa vya uhalifu miongoni mwa vijana," aliongezea Onyagi.