Vijana wanane wameshtakiwa katika Mahakama ya Mombasa kwa madai ya wizi wa mabavu.
Upande wa mashtaka ulielezea mahakama siku ya Jumatatu kuwa vijana hao wanadaiwa kumuibia Margret Charo mali yenye thamani ya shilingi elfu sita wakiwa wamejihami kwa silaha hatari na kutishia kumjeruhi.
Washukiwa hao wanadaiwa kutekeleza kitendo hicho tarehe 15 mwezi Mei, katika eneo la Majengo, Kaunti ya Mombasa.
Aidha, mmoja wa vijana hao, Yassir Hussein, alikabiliwa na shtaka la pili la kupatikana na mali ya wizi.
Washukiwa hao walikana mashtaka hayo mbele ya Hakimu Teresia Matheka.
Hakimu Matheka aliagiza vijana hao kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki moja kila moja.
Kesi hiyo itasikizwa tarehe 16 mwezi Juni.