Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho ameagiza vijana wa kurandaranda mtaani kufurushwa kutoka katikati mwa mji wa Mombasa.
Joho alisema kuwa kuendelea kusalia kwa vijana hao mjini humo kunahatarisha maisha ya wakaazi, hasaa baada ya kubainika kuwa wengi wao huwapora wakaazi nyakati za usiku.
Akizungumza katika hoteli ya Tamarind mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Joho alisema kuwa lazima vijana hao kukusanywa na kurudishwa makwao kama njia moja ya kuimarisha usalama mjini Mombasa, pamoja na kuimarisha shughuli za kibiashara.
Gavana Joho alisema kuwa tayari sekta ya utalii imeanza kuzorota kutokana na hali ya watalii wengi wanaozuru mji huo na maeneo ya kitalii kama vile makavazi ya Fort Jesus kuporwa mali yao na vijana hao.
“Nimeiagiza idara ya askari wa Kaunti ya Mombasa kuwakusanya vijana hao na kuwarudisha makwao ili usalama wa Mombasa uweze ukaimarishwa,” alisema Joho.
Kauli ya Joho iliungwa mkono na wadau wa sekta ya utalii wanaodai kuwa vijana hao na wazazi wao wamekuwa tishio la usalama kwa watalii, hali iliyosababisha sekta hiyo kukumbwa na changamoto.